Chama cha tatu kwa ukubwa wa kisiasa nchini Afrika Kusini, kinachoongozwa na rais wa zamani Jacob Zuma, kimewasilisha hati za kisheria kutaka kusimamisha mkutano wa kwanza wa Bunge uliopangwa kufanyika Ijumaa wa kumchagua rais wa nchi hiyo.
Chama cha Zuma cha Umkhonto weSizwe kimesema hakuna hata wabunge wake 58 waliochaguliwa hivi karibuni watahudhuria kikao hicho. Awali chama hicho kiliwasilisha pingamizi kwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa madai ya kuwepo kasoro nyingi katika uchaguzi wa kitaifa mwezi uliopita. Chama kilipata zaidi ya 14% ya kura.
Chama hicho kinachojulikana pia kama MK, hakijatoa ushahidi hadharani kuunga mkono madai yake. Tume hiyo imesema imeshughulikia mapingamizi yote.
Changamoto hiyo ya kisheria sasa inaitaka Mahakama ya Kikatiba kutengua uamuzi wa tume ya kutangaza uchaguzi kuwa huru na wa haki, na kumwamuru rais kuitisha uchaguzi mwingine.
Uchaguzi huo ulishuhudia chama tawala cha African National Congress kikipoteza wingi wake bungeni kwa mara ya kwanza tangu kuchukua mamlaka miongo mitatu iliyopita mwishoni mwa enzi ya ubaguzi wa rangi.
ANC sasa inataka kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na vyama mbalimbali vya upinzani,
Matokeo ya mazungumzo hayo yataamua ni bunge lipi litamchagua kuwa rais wa Afrika Kusini. Rais Cyril Ramaphosa, mpinzani wa Zuma, anatafuta kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.