Wakati Bajeti Kuu ya Serikali ikitarajiwa kuwasilishwa kesho, Menejimenti ya Tume ya Madini imetakiwa kufanya kazi kwa weledi, umoja na mshikamano ili kufikia lengo la Serikali la makusanyo ya shilingi Trilioni moja kutoka Sekta ya Madini kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba katika ufunguzi wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini jijini Tanga chenye lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa mwaka 2023/2024 na kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji kwa mwaka 2024/2025.
Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Juni 12, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi Bilioni 703.94 sawa na asilimia 79.80 ya lengo walilowekewa la kukusanya kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambalo ni shilingi Bilioni 882.12.
“Kwa mwaka wa fedha unaoisha tumeenda vizuri kwenye makusanyo, haijawahi kutokea, hata hivyo tunapaswa kukaza msuli zaidi ili kufikia lengo la makusanyo ya Serikali tulilopangiwa la kukusanya Shilingi Trilioni moja, kupitia Sekta ya Madini kwa mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai 2024/2025” amesema Mhandisi Samamba.
Aidha, ameitaka Menejimenti ya Tume itoke na mikakati madhubuti ya kuhakikisha inaziba mianya ya upotevu wa mapato.
“Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuweni wakali kuhakikisha mnaziba mianya yote inayokwamisha ukusanyaji mapato ili shida inapotokea kwenye mkoa wako usije kuwajibishwa kwa kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato,”amesema Mhandisi Samamba.
Pia, Mhandisi Samamba amezitaka Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambazo zimeshindwa kufikia lengo kwa mwaka huu unaoisha, zijipange vyema kwa kipindi kilichobaki na mwaka ujao 2024/2025 na kuwataka kuwa wabunifu zaidi ili kuongeza ufanisi kazini bila kusahau kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kusimamia maslahi ya watumishi.
“Tunapaswa kuhakikisha kuwa katika Ofisi tunazozisimamia kunakuwa na hali ya usawa, ushirikiano na maelewano baina ya watumishi kwa ngazi zote,umoja, na ushirikiano ndio iwe nguzo yetu ili kufikia lengo tulilowekewa,” amesisitiza Mhandisi Samamba.