Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima alizikwa Jumatatu kijijini kwake kusini mwa mji mkuu, kufuatia mazishi ambapo Rais Lazarus Chakwera alitoa wito wa uchunguzi huru kuhusu kifo chake katika ajali ya ndege.
Chilima na watu wengine tisa walifariki katika ajali ya ndege wiki iliyopita katika eneo la kaskazini mwa Malawi la Mzimba.
Mazishi hayo ya kiserikali yalifanyika katika Uwanja wa Taifa wa Bingu Bingu mjini Lilongwe Jumapili, ambapo Chakwera na viongozi wengine walitoa heshima zao za mwisho kwa marehemu makamu wa rais.
Katika hotuba yake, Chakwera alitaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu ajali hiyo.
“Machozi yetu yanahusu hamu ya kutaka kujua ni nini kilichelewesha utafutaji wa ndege hii. … Ningependa kuwahakikishia, Wamalawi, kwamba ajali hii itachunguzwa na mtaalamu huru,” Chakwera alisema huku kukiwa na kelele na kejeli kutoka kwa umati.
Mamia ya askari, askari polisi na walinzi wa misitu walikuwa wametafuta kwa zaidi ya saa 24 kabla ya mabaki hayo kugunduliwa katika shamba la msitu kusini mwa Mzuzu.
Ndege hiyo ilikuwa katika safari fupi kutoka Lilongwe kuelekea mji wa kaskazini wa Mzuzu ilipopotea Jumatatu iliyopita asubuhi. Chakwera alisema awali kwamba wadhibiti wa trafiki wa anga waliiambia ndege hiyo isitue Mzuzu kwa sababu ya hali mbaya ya hewa na kutoonekana vizuri na kurejea Lilongwe. Wadhibiti wa trafiki wa anga walipoteza mawasiliano na ndege.