Leo, Jumanne Juni 18.2024 wadau wa sekta binafsi nchini wanakutana kwa ajili ya kujadili mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba Bungeni, jijini Dodoma mwishoni wa juma lililopita
Akitoa hotuba ya ufunguzi wa kikao kazi hicho cha wadau wa sekta binafsi kinachofanyika jijini Dar es Salaam Mkurugenzi mtendaji wa TPSF (Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania) Raphael Maganga amesema baada ya wadau hao kupokea, kupitia na kuchakata mapendekezo ya bajeti hiyo wataandika maazimio ya kikao chao ambapo baadaye maazimio hayo yatafikishwa kwa Waziri husika kama sehemu ya maoni na mapendekezo ya TPSF kwa bajeti hiyo
Amesema miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuangaziwa kwenye mjadala huo ni pamoja na kuona mazingira ya biashara na uwekezaji nchini yanakuwa rafiki, yenye ushindani na yasiyokuwa na vikwazo vya kikodi
Maganga amesema ni wajibu wa kila mmoja kulipa kodi kama ambavyo sheria inaelekeza lakini hata hivyo ni ukweli usiopingika kuwa wafanyabishara na wawekezaji wanahitaji kuona makadirio ya viwango vya kodi yanakuwa rafiki kwao hivyo hilo ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kutazamwa kwa jicho la tatu na serikali kuelekea kwenye utekelezaji wa bajeti kuu ya serikali ya mwaka ujao wa fedha pindi itakapopewa baraka za Bunge
Amesema Tanzania yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 61 ni jambo ambalo halikubaliki kuona hadi sasa kuna idadi ndogo ya Watanzania ambao wanamiliki TIN number, lakini pia ni wananchi wachache wanailipa kodi bila kushurutishwa hivyo ni wakati muafaka sasa kwa serikali kuona namna bora ya kufikia idadi kubwa ya walipa kodi ili mzigo wa kodi usibaki kwa watu wachache ambao wanalazimika kulipa kodi kubwa kama ilivyo sasa.