Mkurugenzi Mkuu wa UDART, Waziri Kindamba leo tarehe 18/06/2024 alifanya ziara na kutembelea vituo vya huduma za Usafiri zinzotolewa na UDART, hii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu na kutaka kujikita zaidi katika maboresho ya huduma za usafiri zinazotolewa na Kampuni ya Mabasi yaendayo haraka UDART.
Mkurugenzi Mkuu, Waziri Kindamba, alianza ziara yake kwa kupitia sehemu za miundombinu ya huduma za BRT ili kuweza kutambua changamoto za usafiri barabarani ambazo mara nyingi zinawakuta Madereva wa Mabasi yaendayo haraka UDART ikiwemo watumiaji wa vyombo binafsi vya usafiri katika miundombinu ya BRT wasio rasmi (Madereva wa pikipiki za abiria Bodaboda na magari bisnafsi yanayopita katika miundombinu ya BRT).
Ziara ya Mkurugenzi Mkuu pia ililenga kufuatilia utoaji huduma katika vituo vya BRT na kuzungumza moja kwa moja na abiria ili kupata maoni yao kuhusu huduma. Mazungumzo hayo vilevile yalilenga kuelewa vizuri changamoto zinazowakabili abiria na kujua jinsi huduma zinavyoweza kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wa huduma za Mabasi yaendayo haraka.
Ziara ya Mkurugenzi Mkuu, Waziri Kindamba ilijumuisha ukaguzi wa huduma katika vituo kadhaa muhimu vya BRT katika jiji la Dar es Salaam. Miongoni mwa vituo alivyotembelea ni pamoja na Kituo Kikuu cha abiria cha Kimara (Kimara BRT Bus Terminal). Kituo cha abiria cha Kimara ni moja kati ya vituo vya BRT vinavyo hudumia idadi kubwa ya abiria kila siku. Mkurugenzi Mkuu Waziri Kindamba alifika Kimara Terminal mapema asubuhi ili kushuhudia shughuli za huduma za asubuhi na kuona jinsi abiria wanavyopata huduma za usafiri.
Mkurugenzi Mkuu katika ziara hiyo alizungumza na abiria waliofika mapema katika Kituo kikuu cha abiria cha Kimara na aliweza kusikiliza maoni ya abiria kuhusu huduma za usafiri, ikiwa ni pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika safari zao za kila siku.
Abiria walitoa maoni yao kuhusu muda wa kusubiri mabasi, ubora wa mabasi na changamoto za kihuduma, na ushauri jinsi ya kuboresha mfumo mzima wa usafiri wa huduma za UDART katika vituo vya BRT.