Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali imeandaa mpango wa mageuzi ya sekta ya mifugo ambao utasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo nchini.
Ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kubuni mbinu na mikakati ya kuondokana na ufugaji usio na tija na kuwezesha kufuga kisasa.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Kibaha, Pwani wakati akifunga Maonesho na Mnada wa Mifugo kwa mwaka 2024.
“ Wizara msichoke wala msiache kuwapa elimu wafugaji wetu, lazima tukubali kuwa wamekuwa hivyo kwa miaka mingi mabadiliko lazima yatokee na lazima tujue kuwa maeneo mengi yanayohitaji ardhi yanaongezeka ikiwa ni pamoja na mifugo lakini ardhi haiongezeki. Hivyo, tuendelee kuwapa elimu ya ufugaji wa kisasa na kuwahimiza wafugaji waje kwenye maonesho kama haya ili wapate ujuzi na teknolojia itakayowasaidia”, amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Wafugaji tujue kwamba nchi na dunia inabadilika ni vizuri tukabadilika sasa kabla mabadiliko yenyewe hayatulazimisha kubadilika kama tumeamua ufugaji ni maisha yetu lazima tuamini maisha yamebadilika tuwe na mifugo yenye tija ambayo itatuletea fedha zitakazoweza kubadilisha maisha yetu.”
Ameendelea kusema “ Wafugaji msijione dhaifu wala wanyonge unaweza kukuta mfugaji ana ng’ombe 1,000 huyo huwezi kumuita masikini, ng’ombe hao wanaweza kuwa mtaji kinachohitajika ni namna gani unaweza kubadilisha maisha yako kwa kutumia hao ng’ombe ulionao.”
Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuboresha sekta ya mifugo nchini ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo huku akiwaasa wafugaji kuepuka kuwa na migogoro baina yao na wakulima kwa kuwa wanategemeana na migogoro hiyo inaathari kijamii na kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa ni vyema maonesho hayo ya mifugo yakafanyika kikanda ili yaweze kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili mfano mbegu bora za mifugo au kujua teknolojia za kisasa za ufugaji.
Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amewapongeza washiriki na wadhamini wa maonesho hayo ya mifugo ambayo yanalenga kutoa elimu kwa wafugaji ili kuleta tija.
“Maonesho haya ni ya muhimu na kwa mwaka huu tumeyawekea nguvu zaidi kwa kuwa yanaleta matokeo makubwa na kwa kuwa yamekuwa maelekezo ya viongozi wetu wa Serikali kuwa wafugaji wetu wasifuge kizamani. Lazima sasa ifike mahali wafugaji wetu waondokane na ufugaji wa kizamani kwa mwamvuli wa kimila, na sisi Wizara tumekuwa tukitoa elimu mara nyingi kupitia wataalamu wetu na Maafisa Ugani licha ya wafugaji hawa kuwa na mwamko mdogo wa kufuga kisasa”, amesema Mhe. Mnyeti.
Ametolea mfano kuwa wafugaji hutembea umbali mrefu kutafuta malisho na matokeo yake mifugo inafika ikiwa imechoka na kuwa Serikali imeendelea kutenga maeneo ya malisho ili kusaidia wafugaji nchini.
“ Tunatoa elimu ya kufuga kisasa kwa kunenepesha mifugo na kuuza hata ng’ombe mmoja kwa shilingi 500,000 au zaidi badala ya shilingi 200,000. Wafugaji lazima wajue ng’ombe ambaye hajafugwa kisasa, hajapata chanjo au akiugua anapewa tu dawa kiholela hawezi kuuzwa nje ya nchi kwa sababu hana ubora”, amesema Mhe. Mnyeti.
Pia, amewataka wafugaji nchini kuwatumia wataalamu wa mifugo ili waweze kupewa elimu ya ufugaji wa kisasa na wenye tija ili kubadilisha sekta ya mifugo nchini.