Kuongezeka kwa ghasia nchini Haiti kutokana na mapigano na magenge yenye silaha tangu Machi kumesababisha karibu watu 580,000 kuyahama makazi yao, kulingana na ripoti mpya kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji.
Haiti kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na machafuko, lakini mwishoni mwa Februari magenge yalianzisha mashambulizi yaliyoratibiwa huku watu wenye silaha wakidhibiti vituo vya polisi, wakifyatua risasi kwenye uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa – ambao ulisalia kufungwa kwa karibu miezi mitatu – na kuvamia magereza makubwa mawili ya Haiti.
Ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, ilisema kuhama kwa zaidi ya nusu milioni kunatokana hasa na watu wanaokimbia mji mkuu wa Port-au-Prince na kuelekea majimbo mengine, ambayo yanakosa rasilimali za kuwasaidia.
Mnamo Machi, shirika hilo liliripoti zaidi ya wakimbizi wa ndani 362,000 nchini Haiti. Ghasia hizo zimeongeza zaidi ya maradufu idadi ya wakimbizi wa ndani katika eneo la kusini – ambalo tayari limeharibiwa na tetemeko la ardhi la 2021 – kutoka 116,000 hadi 270,000.
“Takriban wale wote waliokimbia makazi yao kwa sasa wanashikiliwa na jamii ambazo tayari zinakabiliwa na kulemewa na huduma za kijamii na miundombinu duni, jambo linalozua wasiwasi zaidi kuhusu mvutano unaoweza kuzua vurugu zaidi,” ripoti hiyo ilisema.
Huku zaidi ya watu 2,500 wakiuawa au kujeruhiwa kote Haiti katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka, Polisi wa Kitaifa wa Haiti wameshindwa kudhibiti hali hiyo.