Serikali Mkoani Morogoro imesema Serikali imejipanga kuibua na kukuza vipaji vya vijana na wananchi Mkoani humo hususan katika michezo ikiwemo Riadha, Gofu na Mpira wa Miguu kwa manufaa ya wanamorogoro na taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima wakati akifunga mashindano ya siku ya Olimpiki – Olimpic day yaliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani humo.
“… malengo yetu ni kuwa wawakirishi wazuri wa kamati ya Olimpiki kwa kuzalisha wanamichezo wa aina mbali mbali…” amesema Mhe. Malima
Aidha, Mhe. Adam Malima amesema Mkoa wa Morogoro umeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuweka mazingira mazuri yatakayowasaidia wanamichezo ili kuwezesha Mkoa huo kuwa Mkoa wa Michezo kwani ndani ya wiki mbili kumekuwa na mashindano mawili yakiwemo Mashindano ya Gofu na Siku ya Olimpiki.
Kwa upande wake, Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania Bw. Gulam Rashid amesema maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka ambapo mwaka huu ni mwaka wa 130 tangu kuanzishwa kwake huku ikiwawezesha wachezaji mbalimbali wakiwemo wa riadha katika kufikia malengo mahususi pamoja na kuendeleza vipaji vya wachezaji.
Bw. Gulam ametumia fursa hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Wadau mbalimbali na Wafanyakazi wa Manispaa ya Morogoro kufanikisha usajili wa washiriki zaidi ya 800 waliotoka maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na kufanikisha mashindano hayo.