Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefanikiwa kufikia Halmashauri zaidi ya 60 Nchini katika utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP)
Utekelezaji wa mradi huo unahusisha utambuzi wa kila kipande cha ardhi, Upangaji wa maeneo yote yaliyotambuliwa kwa kuandaa michoro ya mipangomiji, Upimaji wa viwanja vilivyopangwa kwa kuweka alama za upimaji na kuandaa ramani za upimaji na wananchi kumilikishwa maeneo yao kwa kupewa Hatimilki.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita hatimiliki zisizopungua 30,827 zitatolewa kwa lengo la kuboresha milki za ardhi za wananchi ili kuchochea maendeleo ya Wilaya, kuleta usalama wa milki za ardhi, kukukuza uchumi na kupunguza au kumaliza migogoro itokanayo na ardhi.
Hayo yamebainishwa tarehe 27 Juni 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Mhe. Paskasi Muragili wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi wa LTIP katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.
‘‘Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayoongoza na Mhe. Jerry Silaa (Mb.) kwa kuleta mradi huu wenye lengo la kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa Watanzania’’ amesema Muragili.
Aidha Mkuu wa Wilaya huyo aliwaagiza viongozi wote katika Wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa wataalam pindi zoezi hilo litakapoanza pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wanaowasimamia juu ya uwepo wa mradi huu na manufaa yake.
Mtendaji Kata wa Lyambambongo Bw. Jacob Raphael amesema kuwa uwepo wa Mradi huo utasaidia kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi na kupelekea wananchi kupata hatimilki za maeneo yao itakayowasaidia kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.
‘‘Elimu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake ambayo itatolewa itasaidia kuleta mwamko kwa jamii kuhusu umiliki wa ardhi kwa kundi hilo na kupelekea kuwakomboa kiuchumi’’ amesema Raphael.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umejikita zaidi katika kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali katika sekta ya ardhi kwa kuzingatia haki za makundi maalumu kama wanawake, vijana, walemavu, wakulima na wafugaji.