Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa aliteua Baraza jipya la Mawaziri Jumapili jioni baada ya chama chake cha African National Congress, chama kikuu cha zamani cha upinzani, na vyama vingine tisa kukubaliana juu ya muundo wa serikali ya mseto ya utawala wa saba wa Afrika Kusini .
Tangazo la Ramaphosa la Baraza lake jipya la Mawaziri la vyama vingi “lisilokuwa na kifani” limekuja mwezi mmoja baada ya ANC kupoteza utawala wake wa kisiasa wa miaka 30 katika nchi iliyoendelea zaidi kiviwanda barani Afrika katika uchaguzi wa kitaifa, na kulazimisha kutafuta washirika wa muungano.
Mgao wa ANC katika kura ulipungua hadi 40% katika kura ya Mei 29 na kikapoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza tangu kilipoingia madarakani mwishoni mwa mfumo wa ubaguzi wa rangi wa wazungu wachache mwaka 1994.
Chama cha Ramaphosa kilibakia na nafasi kubwa zaidi ya uwaziri alipoteua maafisa wa ANC katika nyadhifa 20 kati ya 32 za Baraza la Mawaziri katika muungano huo mpya.
Lakini kulikuwa na mawaziri sita kutoka chama cha Democratic Alliance, wakati mmoja upinzani mkuu na mkosoaji mkali wa ANC, na Ramaphosa aligawana nyadhifa za mawaziri zilizosalia miongoni mwa baadhi ya vyama vidogo.
DA ilishinda mgao wa pili kwa ukubwa wa kura kwa 21%.