Jeshi la Israel limesema wanajeshi 18 wamejeruhiwa, katika shambulio la ndege isiyo na rubani iliyofanywa na harakati ya Hezbullah ya Lebanon katika milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu.
Katika taarifa iliyotolewa jumapili kwenye akaunti yake ya X, redio ya jeshi la Israel ilisema kuwa majeruhi hao walikuja baada ya “mlipuko wa ndege isiyo na rubani ya Hezbollah iliyorushwa kutoka kusini mwa Lebanon.”
Hizbullah pia ilitangaza kuwa imeyalenga makao makuu ya brigedi ya 91 kaskazini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ili kukabiliana na mashambulizi ya Israel dhidi ya kundi la muqawama la Hezbollah.
Mapema jumapili, Hezbollah ilisema wapiganaji wake watatu waliuawa katika shambulio la anga la Israel lililopiga jengo la ghorofa mbili katika kijiji cha Houla.
Wakati huo huo, jeshi la Israel liliripoti kuwa ndege zake za kivita zilishambulia maeneo ya Hezbollah kusini mwa Lebanon, ikiwa ni pamoja na kituo cha uchunguzi katika eneo la markaba na kiwanja cha kurushia ndege katika kijiji cha Ayta ash Shab.
Hezbollah na Israel zimekuwa zikirushiana risasi mbaya tangu mwanzoni mwa mwezi oktoba, muda mfupi baada ya utawala wa Israeli kuanzisha vita vyake dhidi ya ukanda wa Gaza kufuatia operesheni ya kushtukiza ya kundi la Hamas la Palestina.
Hezbullah imeapa kuendeleza mashambulizi yake ya kulipiza kwa utawala wa Tel Aviv unaendelea na vita vya Gaza ambapo hadi sasa imeua Wapalestina wasiopungua 37,877 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kujeruhi wengine 86,969.
Maafisa wa Hezbollah wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa hawataki vita na Israel lakini ikitokea wako tayari.