Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio aipitisha sheria ya kupiga marufuku ndoa za utotoni, na adhabu ikiwa ni pamoja na vifungo vya jela na faini.
Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio Jumanne alitangaza sheria inayopiga marufuku ndoa za utotoni katika nchi ambayo mamia ya maelfu ya wasichana wameolewa kabla ya kufikisha miaka 18.
“Uhuru umekuja kwa wanawake wetu,” Bio alisema wakati wa hafla iliyoandaliwa na makundi ya wanawake na wake wa marais wa Afrika magharibi katika mji mkuu Freetown.
Bunge la Sierra Leone liliidhinisha sheria hiyo mwezi uliopita, na kupitisha mswada unaoharamisha kuoa wasichana wenye umri wa chini ya miaka 18 na kifungo cha jela cha angalau miaka 15 au faini kali ya zaidi ya dola 2,000.
“Haya ni mafanikio ambayo yatafafanua utawala wangu,” alisema Bio, akiuita “mwanga wa matumaini katika Afrika ambapo wanawake wana fursa zisizo na kikomo za kuwa na kuamua mustakabali wao wenyewe na kuhamasisha ulimwengu.”
Alihimiza nchi “kulea” usawa “kwa kuondoa aina zote za unyanyasaji na maovu ya kutengwa dhidi ya wanawake wetu”.