Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa wanajeshi 1,940 wa Ukraine wameuawa katika muda wa saa 24 huku jeshi la Russia likiendelea kupata nguvu na kusonga mbele zaidi.
Katika taarifa yake, wizara hiyo ilisema wanajeshi 475 wa Ukraine wameuawa katika mapigano na kundi la magharibi la jeshi la Russia.
Jeshi la Ukraine pia lilipoteza wanajeshi 405 katika mapigano na kundi kuu la jeshi, huku wanajeshi wengine 120 wa Ukraine wakiuawa katika mapigano na kundi la mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi 620 wa Ukraine pia waliuawa katika mapigano na kundi la kusini la jeshi la Russia.
Wakati huo huo, kundi la kaskazini liliwalemea wanajeshi wa Ukraine katika maeneo ya mkoa wa Kharkiv na kuzuia mashambulio mawili ya nchi hiyo, sambamba na kuua wanajeshi 320.
Hayo yanaripotiwa baada ya Russia kuanzisha operesheni kubwa dhidi ya eneo la Kharkiv, karibu na maeneo ya mpaka, mwezi Mei mwaka huu.