Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepongeza jitihada zinazofanywa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kupitia mkakati wake wa kujitanua katika mikoa mbalimbali nchini hususani Tanzania Bara, huku Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi akiuomba uongozi wa benki hiyo kufungua tawi lake nchini Msumbiji.
Kwa mujibu wa Rais Samia mkakati wa benki hiyo kuendelea kujitanua katika maeneo mbalimbali nchini hususani kwenye mikoa Tanzania Bara unaifanya benki hiyo iweze kutimiza wajibu wake wa msingi ambao ni kuhudumia wananchi wa pande zote mbili za muungano.
Rais Samia na mgeni wake Rais Nyusi walitoa kauli hizo walipotembelea banda la benki ya PBZ lililopo kwenye viwanja vya Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya SabaSaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam. Wakiwa kwenye banda hilo viongozi hao wawili walipata wasaa kutambulishwa huduma mbalimbali zinatolewa na benki hiyo sambamba na kusikiliza mkakati wake wa kujitanua, zoezi lililooongozwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ Bw Arafat Haji.
“Pamoja na huduma zenu nzuri nimevutiwa zaidi na mkakati wenu wa kuendelea kujitanua katika maeneo mbalimbali hapa nchini hususani mikoa ya Tanzania Bara kwa kuwa hatua hiyo itazidi kuwajenga zaidi kama taasisi iliyo tayari kuwahudumia wananchi wa pande zote mbili za Muungano…hongereni sana’’ alipongeza Rais Samia.
Kwa upande wake Rais Nyusi aliuomba uongozi wa benki hiyo kuangalia uwezekano wa kufungua tawi lake nchini Msumbiji ili iweze kuwahudumia wananchi wakiwemo wafanyabiashara wa mataifa hayo mawili.
“Ni matumaini yangu mkakati wenu wa kujitanua katika maeneo mbalimbali hapa Tanzania unakwenda pia zaidi ya mipaka ya nchi. Hivyo basi nawaomba sana muone namna ambavyo mnaweza pia kuja hadi Msumbiji ili muweze kufungua tawi lenu la kwanza kwa maslahi mapana ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara pande zote mbili,’’ alisema Rais Nyusi.
Awali akitoa ufafanuzi kuhusu huduma za benki hiyo sambamba na mkakati wake wa kujitanua zaidi hapa nchini mbele ya viongozi hao wawili, Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ Bw Arafat Haji alisema benki hiyo yenye matawi 33 ipo kwenye mkakati wa kuongeza matawi zaidi katika mikoa mbalimbali nchini huku akibainisha kuwa tayari benki hiyo imefungua matawi kwenye mikoa ya Morogoro na Mbeya hivi karibuni na pia inatarajia kufungua matawi kwenye mikoa ya Mwanza, Arusha na Tanga.
“Hata hivyo mkakati huu unatoa kipaumbele pia kwenye uwekezaji wa huduma kwa njia za kidigitali ili kuwafikia wananchi kwenye maeneo ambayo bado hayajafikiwa na matawi yetu. Zaidi pia tunatarajia kuzindua ‘Application’ yetu ya simu ambayo tutaizindua rasmi hivi karibuni lengo likiwa ni kuendelea kusogeza na kurahisisha huduma zetu kwa wateja wetu kote nchini,’’ alisema
Akizungumzia ombi la Rais Nyusi la kufungua tawi nchini Msumbiji, Bw Arafat alisema wamelipokea kwa heshima kubwa ombi hilo huku akiahidi kuliingiza kwenye mkakati wao wa utanuzi ili kwenda sambamba na adhma ya benki hiyo ya kuwahudumia wateja wao hata wakiwa nje ya mipaka ya nchi.
“Pia katika kuboresha zaidi uhusiano wetu na serikali tumejipanga kuboresha huduma mbalimbali za serikali ikiwemo huduma yetu ya mfumo wa malipo ya serikali ili kurahisisha na kuchochea kasi ya malipo mbalimbali ya serikali ikiwemo kodi na makusanyo mengine kutoka kwa wananchi kupitia huduma bora za kibenki,’’ alisema.