Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mnamo Ijumaa (Julai 5) alimtuma Mkuu wa Mossad David Barnea kwenda Qatar kwa mazungumzo na wapatanishi juu ya usitishaji vita wa Gaza ambao unaweza kuwafanya wanamgambo wa Hamas kuwaachilia mateka waliokamatwa katika shambulio la Oktoba 7, 2023, shirika la habari la AFP liliripoti likinukuu vyanzo.
Haya yanajiri siku moja baada ya Waziri Mkuu Netanyahu kuitisha mkutano wa baraza lake la mawaziri la usalama kujadili mapendekezo mapya ya Hamas yaliyotumwa kupitia wapatanishi wa Qatar na Misri.
Chanzo kimoja kiliiambia AFP kwamba Mkuu wa Mossad Barnea alitarajiwa mjini Doha siku ya Ijumaa na alitakiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani.
Ujumbe wa Barnea “unasafiri kuelekea Qatar katika muendelezo wa mazungumzo ya kusitisha mapigano na utekaji nyara. Atakutana na waziri mkuu wa Qatar kwa majadiliano yanayolenga kuzileta pande hizo karibu na makubaliano huko Gaza,” chanzo hicho kiliongeza.