Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema Alhamisi (Jul 4) kwamba anaamini kuwa Donald Trump alikuwa mkweli kuhusu kutaka kumaliza vita nchini Ukraine.
Putin aliongezea zaidi kuwa hajui jinsi mgombeaji huyo wa kiti cha urais wa chama cha Republican alipanga kufanya hivyo iwapo atachaguliwa mwaka huu.
Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari nchini Kazakhstan mwishoni mwa mkutano wa usalama wa kikanda, Putin aliulizwa kuhusu matamshi ya Trump kwamba anaweza kumaliza vita vya Ukraine. Urusi inarejelea vita dhidi ya Ukraine kama “operesheni maalum ya kijeshi”.
Putin alisema, “Ukweli kwamba Bw Trump, kama mgombeaji urais, anatangaza kwamba yuko tayari na anataka kusitisha vita nchini Ukraine, tunalichukulia hili kwa uzito kabisa.”
“Bila shaka, sielewi mapendekezo yanayowezekana ya jinsi anavyopanga kufanya hili. Hili ndilo swali la msingi. Lakini sina shaka kwamba anamaanisha kwa dhati, na tunaliunga mkono (wazo la kumaliza vita). “Rais wa Urusi aliongeza.
Wakati wa mjadala na Rais Joe Biden wiki iliyopita, Trump alisema kwamba ikiwa atachaguliwa, mzozo huo “utatuliwa” kabla ya kuchukua madaraka mnamo Januari 2025.
Hii si mara ya kwanza kwani Putin amedai kuwa yuko tayari kwa mazungumzo ya kumaliza mzozo huo. Hata hivyo, mwezi uliopita alidai Ukraine ichukue nafasi hiyo kama sharti la kusitisha mapigano.