Jumla ya washindi 60 wa mbio za NBC Dodoma Marathon msimu huu wanatarajiwa kuondoka na zawadi zenye jumla ya thamani ya Sh. 82 milioni pamoja na medali.
Mbio hizo zenye hadhi ya kimataifa zinatarajiwa kufanyika tarehe 28 Julai mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Lengo la mbio hizo ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.
Hafla ya utambulisho wa zawadi hizo imefanyika leo Ijumaa jijini Dar es Salaam ikihusisha maofisa kutoka benki ya NBC ambayo ndio inaratibu mbio hizo na wadau wa mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo waandishi wa habari.
Tukio limeshuhudiwa na maelfu ya watazamaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyokuwa vikionesha mbashara tukio hilo lenye mvuto wa aina yake.
Wakifafanua kuhusu zawadi hizo Meneja Mahusiano ya Umma na Mawasiliano wa benki ya NBC, Brendansia Kileo na Meneja wa Biashara ya Kadi wa benki hiyo, Esnat Holella wamesema viwango vya zawadi hizo vimeongezwa zaidi msimu wa mwaka huu ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuongeza hadhi ya mbio hizo kila mwaka.
Zaidi ongezeko hilo la viwango vya zawadi linatwaja kuwa linalenga kuchochea ushiriki zaidi wa wanariadha wengi wakiwemo wa kimataifa, hatua ambayo inalenga kuongeza ushindani zaidi kwa washiriki.
“Hivyo, taarifa njema kwa washiriki wa NBC Dodoma Marathon mwaka huu ni kwamba pamoja na medali kwa washiriki wote wa mbio hizi, washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia Sh. 11.5 milioni kila mmoja, Sh milioni tano kwa washindi wa pili, Sh. 2.5 milioni kwa washindi wa tatu, Sh 1.5 milioni kwa washindi wanne na Sh milioni moja kwa washindi wa tano, huku washindi wa sita hadi 10 nao pia wakiibuka zawadi za na pesa taslimu,” amesema Kileo.
Kwa upande wa mbio za Kilomita 21, Kileo amesema pamoja na medali washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia Sh. 5.5 milioni kila mmoja, Sh. 2.5 milioni kwa washindi wa pili, Sh. 1.25 milioni kwa washindi wa tatu, Sh 750,000 kwa washindi wanne na Sh 600,000 kwa washindi wa tano huku pia washindi wa sita hadi wa 10 wakiibuka na zawadi za pesa taslimu kila mmoja.
“Mbio za kilomita 10 washindi wa kwanza wanaume na wanawake watajinyakulia Sh. 2.5 milioni kila mmoja, Sh. 1.5 milioni kwa washindi wa pili, Sh. 750,000 kwa washindi wa tatu, Sh. 500,000 kwa washindi wanne na Sh. 400,000 kwa washindi wa tano, huku washindi wa sita hadi kumi nao pia wakiibuka zawadi za na pesa taslimu,” ameongeza Kileo.
Aidha, Kileo ameongeza kuwa vifaa maalumu vitakavyotumiwa na washiriki wa mbio hizo zikiwemo jezi vinatarajiwa kutolewa kwa washikiri katikati ya mwezi huu .