Katika kusherehekea maadhimisho ya miaka 248 ya Uhuru wa Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), ameishukuru na kuipongeza Marekani kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania huku akiwasihi kukumbuka na kuenzi yale waliyoazimia Julai 4, 1776.
Waziri Makamba amezungumza hayo akihutubia katika hafla hiyo iliyofanyika katika makazi ya Balozi Michael Battle jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Makamba alikuwa mgeni rasmi.
Amewataka Marekani kuwa mstari wa mbele na mfano wa uongozi bora duniani na wenye kulinda amani na kuunganisha watu ili kuiishi taswira ya Dunia yenye haki, isiyo na upendeleo, yenye kujali na isiyo na ubaguzi kama inavyotajwa kwenye Azimio la Uhuru wa Marekani. “Tunatumai, tunatarajia na tunajua kwamba inawezekana kwa nchi hii kubwa ulimwenguni itaendelea kuwa thabiti katika utumiaji wake wa maadili ambayo yanashikilia ubinadamu pamoja,” ameongeza Waziri Makamba.
Aidha, Mhe. Makamba amesisitiza kuwa hakuna nchi inayojitosheleza binafsi na kuwa changamoto za duniani kote kwa sasa zinahitaji ushirikiano na umoja wa kimataifa ili kutatuliwa, huku akipongeza mabalozi kwa kazi nzuri wanazofanya kuziunga nchi zetu
Tanzania na Marekani zimekuwa na ushirikiano wa uwili kwa miaka 63 huku kwa pamoja zikitazamia kuendelea kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zote mbili kwa manufaa ya wananchi wake.