Wabunge nchini Gambia wameidhinisha ripoti ya kamati inayounga mkono marufuku ya mwaka 2015 dhidi ya ukeketaji wanawake, wakati muswada unaotaka kubatilisha sheria hiyo unatarajiwa kupigiwa kura mwisho wa mwezi huu
Ripoti hiyo imeendelea kusema kuondoa marufuku ya ukeketaji wanawake kunawaweka wanawake na wasichana katika hatari kubwa za kiafya pamoja na kukiuka haki yao ya ustawi wa kimwili na kiakili.
Kamati hiyo imesema imeshauriana na wasomi wa Kiislamu waliothibitsha kuwa tamaduni hiyo sio hitaji la Uislamu, hoja ambayo hutumiwa sana na wanaharakati wa ukeketaji.
Baada ya mabishano makali ambayo wakati fulani yalizua kelele, wabunge 35 walipiga kura kuidhinisha ripoti hiyo, huku 17 wakipiga kura ya kuipinga na wawili wakikosa kupiga kura.
Kamati ya pamoja ya afya na jinsia iliwasilisha mrejesho wake Jumatatu ikisema marufuku ya mwaka 2015 dhidi ya ukeketaji wanawake inapaswa kudumishwa kuzuia tohara ya wanawake kwa aina zote nchini Gambia.