Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Santiel Erick Kirumba, amewaomba Wauguzi wa Mkoa Shinyanga kutumia nishati safi ya kupikia badala ya kuni ambazo huzalisha moshi wenye madhara kiafya na pia huaribu mazingira.
Santiel ameyasema leo July 09, 2024 wakati akikabidhi mitungi 200 kwa Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Hospitali ya Manispaa Shinyanga, Kituo cha Afya Kambarage, Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga na Kolandoto, iliyotolewa na Wadau Doris Mollel Foundation pamoja na Kampuni ya uzalishaji gesi (Oryx Gas).
Santiel amesema matumizi ya kuni yamekuwa sababu kubwa ya uharibifu wa mazingira lakini pia huhatarisha afya hususani ya Mama na Mtoto tumboni, sababu si salama, huku akisisitiza kuwepo kwa matumizi mazuri ya gesi ambayo itasaidia kulinda usalama wa afya kwa mama mjamzito.
“Niwaombe Wauguzi, mmekuwa mkipokea Wanawake wengi katika maeneo yenu ya kazi ambao wanaelekea kujifungua, tutumie nishati safi ya kupikia ili kulinda maisha ya Mama na Mttoo, tuachane kabisa na matumizi ya kuni ambayo huhatarisha afya ya Mama mjamzito, licha ya hivyo kuni zinachochea moshi ambao una madhara kiafya, lakini vilevile ukataji wa miti unasababisha jangwa,”
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi hilo kutoka Doris Mollel Foundation, Dorice Laurent, ametoa shukrani kwa kampuni ya Oryx iliyosaidia kupatikana kwa mitungi 200 ambayo itasawadia akina Mama wajawazito katika shughuli mbalimbali za mapishi na kusema lengo lao kama Foundation ni kuhakikisha wanaendelea kugawa mitungi hiyo Nchi nzima ill kuokoa maisha ya Mama na Mtoto, ambao wanakuwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na changamoto ya kiafya, pindi wanapotumia nishati isiyo salama katika shughuli za mapishi.