Mamlaka ya Afrika Kusini imemkamata mwanamume mmoja raia wa Vietnam anayeshutumiwa kwa kujaribu kuuza simba kinyume cha sheria, kundi linalopinga usafirishaji wa wanyamapori lilisema Alhamisi.
Huu Tao Nguyen, 53, alikamatwa na mtu mwingine aliyetambuliwa na polisi kama Nico Scoltz, 32.
Polisi walisema kuwa wawili hao walikamatwa wakati wa operesheni ya siri iliyofuata taarifa kwamba mwanamume mmoja mwenye asili ya Asia alikuwa akiuza simba kinyume cha sheria.
Tume ya Haki ya Wanyamapori yenye makao yake makuu Uholanzi, taasisi inayosaidia mashirika ya kutekeleza sheria kupambana na biashara haramu ya wanyamapori, ilisema Nguyen alijitolea kuuza paka sita wakubwa kwa mawakala wa siri.
Vietnam ni kitovu cha usafirishaji cha wanyamapori haramu.
Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Haki ya Wanyamapori Olivia Swaak-Goldman alielezea kukamatwa kwao kama jambo muhimu.
“Ni matokeo muhimu wakati Afrika Kusini inaelekea kufunga mashamba ya simba ya kibiashara na kuchukua hatua dhidi ya uhalifu unaohusishwa na vituo hivi,” alisema Alhamisi.
Mnamo Aprili, Afrika Kusini iliweka mipango ya kukomesha ufugaji wa simba kwa ajili ya kuwinda huku ikipiga marufuku biashara hiyo yenye utata.