Kampuni zinazojihusisha na uzalishaji wa mitungi ya gesi ya kupikia nchini zimeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini mpango ambao ni endelevu uliozinduliwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wa matumizi ya nishati safi.
Akizungumza na waandishi wa habari Andrew Kashangaki Meneja wa Uwajibikaji kwa jamii kutoka PanAfrican Energy Tanzania ambao wao ni wazalishaji wa gesi ya umeme na magari kutoka kisiwa cha Songo songo amesema katika kuunga mkono juhudi hizi za serikali kampuni imetoa mitungi 500 ambapo mitungi 100 imetolewa mkoa wa Dar es salaam, na mikoa ya Mara 200, Dodoma 100 na Arusha 100
Kupitia tamasha la Samia nishati safi meneja Endrew pia ameelezea changamoto kwa watumiaji wa nishati safi ikiwemo elimu ya matumizi na manufaa kwa jamii hasa kulinda mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia na gharama zake.
“Mpango huu wa nishati safi Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan aliuzindua katika mkutano wa kidunia uliofanyika mwaka jana na amekuwa akiifanya kampeni hii ya kuhamasisha nishati safi ya kupikia.”
“Tupo hapa kutoa elimu na tutaendelea kuwafundisha wananchi ili kuweza kubadilika katika sera hii iliyoanzishwa na rais Samia Suluhu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia”.
“kama PanAfrican Energy Tanzania tutaendelea na programu hii ya kusambaza nishati safi na baada ya tamasha hili tutakwenda kuanzisha mradi katika shule za sekondari 5 katika kisiwa cha Songo Songo wilayani Kilwa na tunatazamia kuhudumia zaidi ya wanafunzi 2000 kwa siku”Meneja Andrew
PanAfrican Energy Tanzania (PAET) imejikita katika kuendeleza na kuzalisha gesi asilia kama nishati salama, safi na yakutegemewa.