Meya wa mji mdogo nchini Ufilipino ambaye ameshutumiwa kuwa jasusi wa China, ameenda mafichoni, maafisa walisema.
Polisi hawakuweza kutekeleza kibali cha kukamatwa kwa Alice Guo mwishoni mwa juma kwa kuwa hakupatikana katika anwani zake zote zinazojulikana.
Vituo vya kulaghai watu vilifichuliwa katika mji wa Bamban mnamo mwezi Machi, vikiwa vimefichwa kwenye kasino za mtandaoni zinazohudumia Wachina wa bara.
Simulizi yake imekuwa kama mchezo wa kuigiza wa televisheni, kwa vile pia aliwahi kuhojiwa kuhusu kuwa mzazi nchini China na tuhuma kwamba alikuwa akifanya kazi kama jasusi wa Beijing.
Bunge la Seneti liliamuru kukamatwa kwa Guo na baadhi ya watu wa familia yake Ijumaa iliyopita baada ya kupuuza mara mbili wito wa kufika kwenye vikao vya kesi inayomkabili.
“Jitokeze. Kujificha hakuwezi kufuta ukweli,” Seneta Risa Hontiveros, anayeongoza uchunguzi wa bunge kuhusu Bi Guo, alisema kwenye taarifa.
Mwanamama huyo amekana kutenda makosa hayo.
Anadai baba yake Mchina na mama yake Mfilipino walimlea kwenye shamba lao la nguruwe.