Beki wa Barcelona Ronald Araujo huenda akapigwa marufuku na FIFA kwa kuhusika katika pambano kati ya wachezaji wa Uruguay na mashabiki wa Colombia.
Machafuko yalitokea baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa katika nusu-fainali ya pili ya Copa America 2024 huku wachezaji wa Uruguay wakionekana kuruka uwanjani kukabiliana na wafuasi wa Colombia.
Nyota wa Liverpool, Darwin Nunez alionekana kuwa katikati ya tukio hilo huku Araujo wa Barcelona pia akiwa miongoni mwa wachezaji waliohusika katika matukio hayo machafu.
Kutokana na hali hiyo, wababe hao wa Catalan wanahofia kwamba beki huyo wa kati anaweza kupigwa marufuku na FIFA, kwa mujibu wa Diario AS. Ripoti hiyo inaongeza kuwa Araujo anatazamiwa kurejea Barcelona kufanyiwa vipimo vya afya kutokana na jeraha la msuli wa paja alilopata akiwa kwenye majukumu ya kimataifa.
Ingawa vipimo vipya vya matibabu vitaonyesha ukubwa wa jeraha la mchezaji huyo, ripoti za mapema zilipendekeza kwamba anaweza kukosa mechi chache za mwanzo za msimu wa 2024-25.