Kylian Mbappé, nyota wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa, ameweka rekodi mpya kwa kukusanya mashabiki 80,000 waliojitokeza kwenye sherehe za utambulisho wake katika klabu hiyo. Sherehe hiyo ilifanyika katika uwanja wa nyumbani wa Real Madrid, Santiago Bernabeu.
Rekodi hii mpya inalingana na ile iliyowekwa na Cristiano Ronaldo mwaka 2009, ambapo naye alikusanya mashabiki 80,000 kwenye utambulisho wake. Hii inaonyesha kuwa Mbappé ana ushawishi mkubwa sawa na Ronaldo katika ulimwengu wa soka.
Nyota wa Ufaransa Kylian Mbappe alitambulishwa rasmi kama mchezaji wa Real Madrid Jumanne, na kuwaambia mashabiki 80,000 “ndoto yangu imetimia”.
“Nimelala kwa miaka mingi nikiwa na ndoto ya kuichezea Real Madrid na leo ndoto yangu imetimia,” Mbappe aliwaambia mashabiki waliokusanyika kwa wingi kumlaki katika uwanja wa Santiago Bernabeu wa klabu hiyo.
Mshambulizi huyo, ambaye alikuwa amekamilisha vipimo vyake mapema Jumanne asubuhi, alisaini mkataba wa miaka mitano na kukabidhiwa jezi nambari 9 na rais wa klabu Florentino Perez.
Akiwa ameambatana na wazazi wake waliokuwa wakitazama kutoka kwa umati wa watu na gwiji wa zamani wa Ufaransa wa klabu hiyo, Zinedine Zidane, aliyehudhuria, Mbappe alijawa na hisia huku umati wa watu wakiimba jina lake, na wakati fulani akabusu jezi ya mabingwa hao watetezi wa Uhispania na Ulaya.