Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imezidua huduma ya bima kupitia benki (Bancassurance) ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo kuboresha zaidi huduma zake sambamba na kuongeza ujumuishaji wa jamii zaidi katika mfumo rasmi wa fedha kupitia huduma za bima.
Zaidi hatua hiyo inatajwa kuwa inalenga kuunga mkono jitihada za serikali kupitia Mpango Mkakati wa Fedha wa miaka kumi (2020 -2030) unaolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya watanzania wana uelewa wa kutosha kuhusu huduma za bima huku asilimia 50 wakiwa wanatumia huduma za bima.
Hafla ya utambulisho wa huduma hiyo ilifanyika jana Zanzibar ikiongozwa na Naibu Kamishna wa Bima Tanzania, Bi Khadija Said na kuhuduriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya bima na wateja. Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ, Bw Arafat Haji aliwaongoza wafanyakazi wengine wa benki hiyo kwenye hafla hiyo muhimu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bi Said pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo muhimu alisema huduma hiyo itasaidia kuchochea kasi ya utoaji wa huduma za kibima visiwani humo na nchi nzima kwa ujumla huku pia ikitoa fursa nyingi za kiuchumi kupitia hakikisho la usalama wa mali za wananchi hususani waliopo pembezoni.
“Hatua hii ya PBZ ni muhimu sana kwetu serikali kwa kuwa inaunga mkono utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Fedha wa miaka kumi (2020 -2030) unaolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 asilimia 80 ya watanzania wana uelewa wa kutosha kuhusu huduma za bima huku asilimia 50 wakiwa wanatumia huduma za bima.” Alibainisha huku akitoa wito kwa benki hiyo kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa huduma za bima kupitia benki.
Aidha Bi Said alitoa wito kwa taasisi za fedha nchini kuendelea kushirikiana na kampuni mbalimbali ya bima ili kwa pamoja waweze kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu sambamba na kubuni mikakati bora zaidi ya masoko ili kuendelea kubuni mikakati bora zaidi ya kuwafikia wananchi kupitia huduma zinakidhi mahitahi yao.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Bw Haji alisema ujio wa huduma hiyo yenye baraka zote kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo kuendelea kuboresha huduma zake huku dhamira ikiwa ni kutoa huduma zote katika sehemu moja (One Stop Shop).
“Huduma hii itatolewa kupitia matawi yote ya PBZ yaliyopo kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kushirikiana na makampuni mbalimbali ya bima kama ilivyoidhinishwa na TIRA. Kupia hatua hii sasa PBZ tumejipanga kuwawezesha wateja wetu kupata huduma za bima pamoja na huduma nyingine za kifedha kama vile kupata mkopo kwa ajili ya malipo ya bima(Insurance Premium Financing) katika kiwango cha ushindani.” Alibainisha.
Alizitaja huduma za bima zinazotolewa kupitia huduma hiyo kuwa ni pamoja na Bima za Maisha, Bima kwa Vyombo vya Moto, Bima za Wanajenzi (Engineering Insurance), Bima za Moto, Bima ya Madeni (Liability/Third Party Liability Insurance), Bima kutokana na wizi (Burglary Insurance) na Bima ya Afya.
“Huduma nyingine ni pamoja na Bima kutokana na Mfanyakazi asiyekuwa muaminifu (Fidelity Guarantee), Bima ya Pesa, Bima ya Vyombo vya Baharini, Dhamana (Bond Insurance and Counter Guarantees), na Dhamana za mali ambazo hazikutolewa katika mkataba wa Bima (Asset All Risk Insurance),” alitaja.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara wa benki hiyo Bw Eddie Mhina alitaja kampuni za Bima zilizohusishwa kwenye mpango huo kuwa ni pamoja na Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Shirika la Taifa la Bima (NIC), Alliance Life, Jubilee Insurance, Strategis Insurance na Metro Life Assurance.
“Uzinduzi wa mpango huu umekuja wakati PBZ tunaendelea kufanya vizuri kupitia huduma zetu za kidigitali na hivyo kuendelea kutambuliwa kama moja ya taasisi za kifedha zinazotekeleza vema adhima ya Benki Kuu ya Taifa (BoT) katika kufikia uchumi jumuishi wa kidigitali na kuelekea kwenye uchumi usiotegemea zaidi matumizi ya pesa taslimu (cashless society).” Aliongeza Mhina.
Kwa mujibu wa Bw Mhina lengo la benki hiyo kuondoa usumbufu kwa wateja kwa kuongeza nyongeza kadhaa za thamani kwenye huduma ya bima ikiwemo ufikiaji rahisi wa kuripoti madai, urahisi katika kusajili bima mpya ambapo wateja watapewa taarifa za kuisha kwa kipindi cha bima zao kidigitali sambamba na kupatiwa msaada wa karibu katika kusajili bima upya.
Mwisho.