Tume ya kitaifa ya haki za binadamu nchini Kenya, imesema idadi ya watu waliokufa kutokana na maandamano yaliyoanza mwezi uliopita imefikia 50 baada ya hapo jana watu wawili kuripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano mapya ya kutaka rais William Ruto, aachie ngazi.
Karibu siku nzima, polisi walitumia mabomu ya machozi kuwasabaratisha waandamanaji, waliokusanyika katikati ya jiji la Nairobi.
Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Idara ya Huduma kwa Polisi Jumanne ilitoa taarifa ya tahadhari kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanyika Julai 17.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa Jumanne asubuhi, Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi, Douglas Kanja Kirocho alibainisha kuwa baadhi ya makundi ya wahalifu yanapanga kujipenyeza na kuvuruga maandamano hayo ya amani, hatua ambayo inaweza kuvuruga amani na usalama wa waandamanaji.
“Hata hivyo, katika kipindi cha hivi majuzi, tumeshuhudia kwa masikitiko makubwa vifo vya watu, majeraha, vurugu, uhalifu na uharibifu wa mali kutokana na maandamano ya aina hiyo, na kusababisha uchungu na mateso kwa familia na kuvurugika kwa biashara na shughuli za kawaida za kufanya kazi. maelfu ya Wakenya.