Sheikha Mahra bint Mohammed bin Rashid Al Maktoum ambae ni binti yake Mtawala, Makamu wa rais na Waziri mkuu wa Dubai Sheikh Mohammed Bin Rashid Al Maktoum amezua gumzo mitandaoni baada ya kutangaza kutalikiana na mume wake kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram akimshutumu mume wake kujihusisha na wanawake wengine.
Binti Mfalme huyo alitangaza kufikia tamati kwa ndoa yake na Sheikh Mana bin Mohammed bin Rashid bin Mana Al Maktoum ambae ni mfanyabiashara kutoka jijini Dubai miezi miwili baada ya kumkaribisha mtoto wao wa kwanza.
“Kwasababu umejihusisha na wanawake wengine, ninatangaza talaka yetu. Ninakupa talaka, ninakupa talaka, na ninakupa talaka,” aliandika, akionekana kumpatia mume wake talaka tatu ikiwa ni moja ya utaratibu unaotumika kwa miaka mingi nchini humo ambapo wanaume wa kiislamu wanaweza kuwataliki wanawake waliowaoa kwa kudhihirisha nia yao mara tatu kwa kutumia maneno.
Kwa mujibu wa taarifa, sio jambo la kawaida kwa mwanamke kutoa talaka tatu chini ya sheria za Kiislamu, ambayo inasema kwamba wanawake wanaweza kuomba talaka kwa utaratibu unaoitwa “khula” ikimhusisha mwanamke aliyeolewa kuwasilisha ombi rasmi mahakamani na kutaja sababu halali ya maombi ya talaka.