Mkufunzi wa Newcastle Eddie Howe amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kuinoa timu ya taifa ya Uingereza baada ya kuhusishwa pakubwa na nafasi hiyo mpya iliyoachwa wazi.
Howe alijibu tetesi za meneja huyo wa Uingereza wakati wa mahojiano na Sky Sports alipokuwa kwenye kambi ya Newcastle ya kujiandaa na msimu mpya nchini Ujerumani. Lakini aliweka wazi kwamba kupata mafanikio na Magpies ni kipaumbele chake pekee na kitu kingine chochote – ikiwa ni pamoja na Uingereza – “sio muhimu”.
Howe amekuwa mmoja wa majina ya awali yanayohusishwa na kibarua cha Uingereza pamoja na kocha wa zamani wa Chelsea Graham Potter. Amekuwa akipendekezwa kama meneja wa baadaye wa England tangu wakati wake huko Bournemouth. FA sasa wamechapisha tangazo la kazi kwa umma, wakiorodhesha vigezo saba muhimu wanavyotaka wagombeaji watimize.