Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Chilo amezindua na kushiriki zoezi la upandaji miti kando kando mwa Mlima Kilimanjaro ili kupunguza kasi ya kuyeyuka kwa barafu ya mlima huo mrefu duniani kutokana na mabadiliko ya Tabianchi yanayoikumba dunia kwa sasa.
Akizundua Kampeni ijulikanayo kwa jina la “Save Mount Kilimanjaro yenye matarajio ya kupanda miti zaidi ya bilioni 1 kwa mikoa ya Kaskazini yenye mchango kwenye mlima huo Chilo alisema, “ Mlima Kilimanjaro ni moja ya tunu za Taifa, hivyo upandaji wa miti hii utasaidia kuokoa barafu ya Mlima huu ambao umeendelea kivutio kikubwa kwa watalii kuja kupanda na kuishuhudia barafu hiyo”.
“Niwapongeze Taasisi ya Nessa Foundation kuja na Kampeni hii itakayosaidia kuimarisha Ikolojia ya Hifadhi yetu ya Kilimanjaro, pia utapandaji wa miti hii utaongeza kiasi cha mvua kwa mikoa hii ya Kaskazini na kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi,” aliongeza Mhe. Chilo.
Ikumbukwe kuwa watabiri na watafiti mbalimbali walibashiri kuwa ifikapo 2050 barafu ya Mlima Kilimanjaro iliyopo katika kilele cha Uhuru mita 5895 itatoweka, hivyo upandaji wa miti hii utasaidia kuongeza barafu hiyo na kupunguza hewa ya Ukaa ambayo ni kichocheo kikubwa cha joto duniani. Joto hilo limekuwa na matokea hasi ya kuongeza kasi ya uyeyukaji wa barafu hiyo.
Sambamba na upandaji miti pia, Mhe. Chilo amewataka baadhi ya watanzania wenye tabia na desturi ya kuvamia maeneo yaliyohifadhi kwa ajili ya kujihusisha na shughuli za kibinadamu kuacha mara moja kwani mbali na kuharibu maliasili pia kutaathiri sekta nzima ya utalii.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Nessa Foundation Bi. Deborah Nyakisinda alisema, “Tunaishukuru (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na wadau wote walioshiriki katika kampeni hii ya kupanda miti ili mikoa hii iwe ya kijani.”
Kamishana Msaidizi wa Uhifadhi, Maendeleo ya Biashara TANAPA – Jully Lyimo aliwapongeza wadau wote kwa kujitokeza kuunga mkono juhudi za kupanda miti ili kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro.
“Tukio hili lina sura ya kulinda mazingira kwa sababu leo tumepanda miti na tumefanya utalii wa ndani, niwakaribishe Watanzania na wasio Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa, aidha niwaase kuendelea kutunza mazingira ya Mlima huu ili uendelee kuwa kivutio bora Afrika na dunia kwa ujumla,”aliongeza Kamishna Lyimo.
Naye, Afisa Uhifadhi Mkuu Mapinduzi Mdesa ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro alihamasisha hadhira hiyo kuupigia kura Mlima Kilimanjaro ambao unawania tuzo za World Travel Awards katika kipengele cha Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika kwa mwaka 2024 (Africa’s Leading Tourist Attraction 2024).
Zoezi hilo la upandaji miti lililozinduliwa jana Julai 20, 2024 lilitanguliwa na matembezi mafupi ya kilometa 5 ili wananchi hao kujiweka tayari na kuwa na utimamu wa mwili kwa ajili ya zoezi hilo, huku mikoa itayofaidika na miti hilo ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara.