Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema upo umuhimu mkubwa wa ushirikiano na ubadilishaji uzoefu kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika kupeana uzoefu wa kutatua changamoto zitakazoibuliwa katika kutoa Mafao ya Wafanyakazi wanaoumia kazini au kupata ugonjwa unaotokana na kazi zao.
Amesema hayo baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa mashirikiano (MoU), baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), katika nyanja mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yao .
Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma na Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF, Nassor Shaaban Ameir na hafla ya utiaji sahihi imefanyika Mjini Unguja, sanjari na ufunguzi wa kikao kazi baina ya WCF na Divisheni za Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Mahakama Kuu ya Zanzibar ambacho pamoja na mambo mengine kimejadili Sheria za Haki Kazi.
Akiongea kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Kiongozi, Mustapher Siyani amesema “Imani ya Wawekezaji haiwezi kukamilika kama mfumo wa utoaji haki haujaimarishwa, Wawekezaji wanataka uhakika wa mfumo wa utoaji haki utakaolinda maslahi yakiwemo ya Waajiri na Waajiriwa”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema, hatua hiyo ni uthibitisho wa mahusiano imara na ya muda mrefu baina ya Taasisi hizo huku Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF, Nassor Shaaban Ameir akisema, Mfuko huo umeanzisha fao la FIDIA SKIMU kwa ajili ya kuwafidia Wafanyakazi wanaopata ajali na magonjwa wakiwa kazini.
.