Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewaonya watakaoandamana nchini humo kwamba watakuwa “ wanacheza na moto” ikiwa wataendelaa na mipango yao ya kufanya maandamano dhidi ya ufisadi hadi bungeni siku ya Jumanne Julai 23.
Vijana nchini Uganda wamekuwa wakiandaa maandamano kwenye mitandao ya kijamii wakitaka ufisadi kumalizwa serikalini.
Wameshawishika na maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika katika nchi jirani ya Kenya, ambapo vijana wenzao wamekuwa wakiandaa maandamano ambayo yalimlazimu Rais William Ruto kusitisha mipango ya kuongeza kodi.
Katika taarifa iliyorushwa kwenye runinga nchini Uganda, Rais Museveni aliwaonya waandaaji kwamba mpango wao wa kufanya maandamano hautakubalika wala kustahmiliwa.
“Tuko mbioni tukijaribu kuzalisha mali…Nanyi mnataka kutusumbua. mnacheza na moto kwa sababu hatutakubali mtusumbue,” alisema.
Rais Museveni amelaumiwa na wakosoaji wake kwa kuingoza Uganda kiimla, tangu kuchukua mamlaka mwaka 1986, lakini wafuasi wake wamempongeza kwa kudumisha amani katika taifa hilo la Afrika Mashariki.
Rais huyo pia amewashutumu wanaopanga maandamano hayo kuwa “wanashirikiana na mashirika na watu kutoka mataifa ya kigeni” kuleta vurugu nchini Uganda. Ila hakueleza zaidi kuhusu madai hayo.
Polisi nchini humo, hapo awali walikuwa wametangaza kwamba walikata kutoa idhini kwa watu waliotaka kuandamana hadi nje ya majengo ya bunge siku ya Jumanne.
Mmoja wa viongozi wa maandamano hayo aliambia kituo cha Habari cha AFP kwamba wataendelea na mpango wao.