Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kwamba, taifa hilo linakabiliwa na “kuongezeka kwa kasi” kwa idadi ya wagonjwa wa Homa ya nyani, Mpox.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya amesema kuwa, idadi ya wanaoshukiwa kupata maambukizi ya homa hiyo imefikia watu 11,166, ikiwa ni pamoja na vifo 450.
Afisa huyo wa serikali ya DRC amesema, ripoti ya wizara ya afya imefichua ongezeko kubwa la idadi ya visa vya maambukizi, huku mkoa wa magharibi wa Equateur ukiathirika zaidi.
Aidha ripoti hiyo imesema serikali inachukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo, hasa katika huduma ya matibabu, ufuatiliaji wa maeneo husika ya afya na kuongeza ufuatiliaji miongoni mwa jamii.
Haya yanajiri siku chache baada ya Shirika la Afya Duniani kuonya juu ya tishio la afya duniani linaloletwa na ugonjwa wa huo “Mpox” huku kukiwa na wasiwasi wa uwezekano wa kutokea mlipuko wa aina mpya ya virusi hatari zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2022, baada ya mfululizo wa mashauriano na wataalamu wa kimataifa, hatimaye shirika la Afya la Afya Duniani ( WHO) lilianza kutumia jina MPOX badala ya Monkeypox au Homa ya Ndui na Homa ya Nyani kwa maelezo ya kwamba lilikuwa linasababisha mambo kadhaa ikiwemo unyanyapaa.