Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa Taasisi zote zinazotoa huduma za kijamii kama shule na vituo vya afya pamoja na nyumba za ibada zitafikishiwa umeme.
Naibu Waziri Kapinga ameyasema hayo leo Julai 22 wakati akiwasha umeme katika Shule ya Sekondari Nyasa iliyoko katika Kijiji cha Chimate wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.
“Sisi kama Wizara ya Nishati ni kuhakikisha tunaongeza tija katika taasisi hizi zinazotoa huduma kwa kufikisha umeme. Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anahangaika usiku na mchana kutafuta fedha za kuboresha maisha ya Watanzania kila siku na kazi yetu kubwa ni kuhakikisha taasisi na maeneo yote yenye umuhumi yanafikiwa na umeme.
Tayari TANESCO na REA wamejidhatiti maeneo ambayo kuna taasisi za kijamii kama shule, vituo vya afya, makanisa, misikiti vyote vinafikiwa na umeme ili kuboresha huduma za kijamii katika Taifa letu,” amesema Naibu Waziri Kapinga.
Amesema kuwa uwepo wa umeme shuleni umesaidia hata kuongeza ufaulu kwa kuwa wanafunzi wamekuwa wakipata muda wa kujisomea hata usiku tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya miradi ya kusambaza umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) haijaanza.
Awali akitoa taarifa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Eng. Robert Dulle amesema kuwa gharama za kufikisha umeme katika kijiji hicho ni shilingi Milioni 286.
Eng. Dulle ameongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma unajumla ya Vijiji 554 na mpaka kufikia Julai 2024, vijiji 542 sawa na asilimia 97.8 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi inayotekelezwa na REA na kwa Wilaya ya Nyasa kuna jumla ya vijiji 84 ambapo vyote vimepata umeme.
Eng. Dulle pia amewahamasisha wananchi kuchangamkia fursa za uwepo wa umeme vijijini kufanya shughuli za kiuchumi zitakazoboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyasa, Mwalimu John Ndelwa ameipongeza REA kwa kuwafikishia umeme shuleni kwao na kuahidi kuwa watatumia fursa ya kuwepo umeme kuwafundisha wanafunzi masomo ya jioni na hivyo kuongeza ufaulu.
Ameongeza kuwa uwepo wa umeme utawawezesha kuwa na mitihani mingi ya majaribio kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kuchapa mitihani wenyewe shuleni tofauti na awali ambapo walikuwa wanalazimika kutumia gharama kubwa kwenda kuchapisha katika steshenari