Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson amezindua rasmi tawi la Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkoani Mbeya huku akiwaomba wananchi kutumia taasisi rasmi kupata huduma mbalimbali za kifedha hususani kipindi hiki ambacho Bunge kwa kushirikiana na serikali wanaandaa sera bora zaidi zitakazosimamia huduma ya fedha nchini.
Hafla ya uzinduzi wa tawi hilo lililopo eneo la Mafiati jijini Mbeya imefanyika mapema leo Jumanne ikiongozwa na Spika Dk. Tulia aliyewaongoza wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa chama na serikali kutoka pande zote za Muungano, viongozi wa dini, wawakilishi wa wafanyabaishara jijini humo na maofisa wa benki hiyo wakiongozwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki hiyo Arafat Haji.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma alimuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Dk. Saada Mkuya Salum.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Dk. Tulia pamoja na kuipongeza benki ya PBZ kwa kuendelea kujitanua zaidi hapa nchini ikiwemo kwenye jiji hilo, aliwaomba wananchi kutumia zaidi taasisi rasmi za kifedha kupata huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo kujiwekea akiba na mikopo ili wanufaike na faida mbalimbali za taasisi hizo ikiwemo kupata elimu ya fedha kuhusu faida ya kujiwekea akiba na matumizi sahihi ya mikopo wnayochukua.
“Uhimu wa kutumia taasisi rasmi za kifedha ni mkubwa na hata marejesho yake yanafanyika kwa utaratibu mzuri tena bila riba za kinyonyaji kuliko mikopo inayotolewa na taasisi zisizo rasmi ambazo kwanza hazifuati utaratibu na riba zake ni kubwa zinazolenga kuwanyonya wananchi.
“Mikopo hii isiyo rasmi siku hizi zinazotolewa kwa njia ya simu bila utaratibu na matokeo yake huwa ni kuwatapeli wananchi na kuleta usumbufu mkubwa si kwa waliokopa bali pia hata watu wao wa karibu kwasababu huwa wanatumiwa meseji zenye nia ovu ya kudhalilisha wakopaji,” alisema.
Hata hivyo Dk. Tulia alisema Bunge linaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha sekta ya fedha nchini inaongozwa na sera bora zaidi ambazo zitawavuta zaidi wananchi kufuata huduma za kifedha kwenye taasisi rasmi ikiwemo kutazama vizuri suala zima la riba zinazotolewa na taasisi rasmi. Zaidi alisema Bunge linashirikiana vema na serikali kuhakikisha wanakabiliana na taasisi zisizo rasmi kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumzia tawi hilo, Dk. Tulia alisema ujio wake mkoani humo ni matokeo ya ukuaji wa uchumi, ubora wa miundombinu pamoja na sera nzuri za uwekezaji unaovutia wadau mbalimbali mkoani humo.
Aidha, aliwaomba viongozi wa PBZ kuhakikisha huduma zao zinagusa makundi yote ya wananchi kwa vigezo vya umri, jinsia na uchumi binafsi huku kipaumbele kiwe ni kuwasaidia vijana kupitia mikopo rafiki yenye kulenga kuwasaidia kiuchumi kupitia biashara zao na kilimo.
Kwa upande wake Waziri Riziki alisema ujio wa tawi la benki hiyo mkoani humo ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayomiliki benki hiyo kwa asilimia 100 pamoja na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Riziki aliwaomba wananchi wa mkoa huo kutumia ujio wa benki hiyo kama mwamko wa wao kufungua fursa za kibiashara na kilimo kati ya mkoa huo na Zanzibar.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya PBZ, Arafat Haji alisema hatua ya kufungua tawi hilo mkoani Mbeya ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo kuendelea kujitanua mikoa mbalimbali hapa nchini huku pia ikitimiza wajibu wake wa msingi wa kufungua fursa za kiuchumi miongoni mwa wananchi wa pande zote za muungano.
“Tawi hili litafungua zaidi fursa za kibiashara kwa wananchi mkoani hapa lakini pia litafungua milango ya mahusiano ya kibiashara baina ya wakazi wa Mbeya na Zanzibar kwa kuangazia fursa zilizopo pande hizi mbili ikiwemo kilimo na biashara. Huduma zetu ni rafiki zaidi kwa makundi yote na niimani yangu zitawavutia zaidi nawakaribisha sana waje wajionee tofauti,” alisema.
Kufuatia ombi la Dk. Tulia, kwa niaba ya benki hiyo, Arafat aliahidi kutoa msaada wa pikipiki 10 ili kuunga mkono jitihada za mbunge huyo katika kuwasadia vijana hususani waendesha pikipiki.
Akitoa salamu za mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Benno Malisa aliemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo alisema ongezeko la taasisi za fedha mkoani humo ni ishara njema ya ukuaji wa uchumi na uwepo wa mazingira bora ya biashara na uwekezaji na hivyo kuiomba benki hiyo kuwa sehemu ya chachu ya kuchochea maendeleao hayo kupitia utoaji wa mikopo ya kibiashara na kilimo.