Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewataka Wasimamizi na Watendaji wa bonde la Wami – Ruvu kutimiza wajibu wao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kuhakikisha mazingira ya Bwawa la Mindu ambalo ni roho ya Wananchi wa Morogoro yanakuwa sawa.
Amesema hayo leo Tarehe 23 Julai 2024 akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Morogoro; ambapo anakagua mitambo ya kusukuma maji Tumbaku, kukagua shughuli za uzalishaji maji Mafiga, kushuhudia utiaji saini mkataba wa uboreshaji wa huduma ya maji – Gairo na kuongea Wananchi.
Amesema Bwawa hilo ambalo ni chanzo kikuu cha maji likitetereka litawaweka Wananchi katika mtihani; hivyo ameagiza wahusika kuweka nguvu zaidi katika kulinda na kutunza wa vyanzo vya maji kwa sababu kwenye eneo hilo majani yamesogea mpaka kwenye Bwawa.
Amesisitiza kuwa “hauwezi ukaruhusu majani yamefika mpaka kule na leo tumekuja tumekuta watu wanakata katakata, jambo la pili tumeona makazi ya watu yanazidi kusogea katika chanzo hiki kikuu cha maji, nafikiri tushirikiane sasa, hii sio kazi ya mtu mmoja, na nyie mkubali pia kushirikisha kwa sababu jamii ipo, na Viongozi wapo usipowashirikisha utakwama tu”.