Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC, Nah. Mussa Mandia ameielekeza TPA kuweka utaratibu mzuri wa abiria kuingia kwenye meli, kujenga jengo la kutunzia mizigo na kutenganisha mizigo ya vyakula na mizigo mengine katika Bandari ya Nyamisati.
Hayo ameyabainisha leo wakati akizungumza na vyombo vya habari kwenye baada ya ziara ya ukaguzi katika bandari ya Nyamisati iliyopo wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
“Hongereni sana mnafanya kazi nzuri na tumeridhishwa na utekelezaji wake ila mngeweka utaratibu mzuri wa abiria kuingia kwenye meli, mjenge jengo la kutunzia mizigo na kutenganisha mizigo ya vyakula na mizigo mengine hiyo itawezesha kusaidia kuondokana na Changamoto zisizo za lazima”. Amesema Mandia
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohamed Salum amesema “bandari hii ni ndogo lakini inafanya vizuri katika kutoa huduma za usafiri, Bodi imetuelekeza tuendelee kusimamia uboreshaji wa eneo la bandari lenye udongo linalolika kwa maji kwa kuwekwa tabaka gumu ili maji yasiendelee kuondoa udongo”
Naye Meneja wa bandari Nyamisati, Issa Unemba amesema kuwa bandari hii ni ya kimkakati katika kuhudumia visiwa vya bahari Hindi. Hivyo wamefanya maboresho mengi bandari hapo na wataendelea kuboresha zaidi kwa kuwa vifaa vya kupakia na kupakua mizigo.
Bandari hii inahudumia meli tatu, na vyombo vidogo vya usafiri majini.Kwa mwaka inasafirisha abiria zaidi 4000 na mizigo zaidi ya tani 200 kwa mwezi.