Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa lina wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kutokea mlipuko mkubwa wa polio huko Ukanda wa Gaza kufuatia kugunduliwa hivi karibuni virusi vya polio kwenye maji taka.
Ayadil Saparbekov mkuu wa timu ya WHO inayoshuhughulikia dharura za kiafya huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ameuambia mkutano wa Umoja wa Mataifa huko Geneva kwa njia ya video kutoka Ukanda wa Gaza kwamba ana wasiwasi mkubwa kuhusu mlipuko wa polio (ugonjwa wa kupooza viungo vya mwili) unaoweza kutokea katika ukanda huo.
Shirika la Afya Duniani limeripoti kuwa virusi vya polio aina ya pili vimegunduliwa katika sampuli zisizopungua sita za maji taka zilizokusanwa katika Ukanda wa Gaza. Sampuli hizo zimekusanywa katika maeneo mawili tofauti yaani katika mji wa Khan Yunis kusini mwa Gaza na huko Deir al Balah katikati mwa ukanda huo.