Leo July 26,2024 imeitwa tena kwa mara ya tatu kesi ya watuhumiwa tisa wa mauaji ya mtoto Asimwe Novart aliyekuwa na ualbino ambaye alichukuliwa nyumbani kwao Kamachumu may 30 mwaka huu 2024 ambapo June 17 mwaka huu 2024 mwili wake ulikutwa kwenye kalavati akiwa ameuawa na kukatwa baadhi ya viungo vyake.
Watuhumiwa hao tisa wamefikishwa tena katika mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba kwa ajili ya kutajwa tena shtaka lao
Wakili wa serikali Erick Mabagala amesema kuwa bado wanaendelea kushughulikia utaratibu wa kusajili shauri hilo katika mahakama kuu ambayo ndo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia na uchunguzi wa shauri hilo no 17740 la mwaka 2024 tayari umekamilika.
Shauri hilo limeitwa tena mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba Elipokea Yona Wilson ambaye amesema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na wamerudishwa rumande mpaka August 9,2024 ambapo kesi yao itatajwa tena huku wakisubili kukamilishwa jalada lao.
Watuhumiwa hao tisa ni Elpidius Alfred Rwegoshora miaka 49 ambaye ni padri,Novat Venant miaka 24 ambaye ni baba wa mtoto Asimwe,Nurdin Ahmada,Ramadhan Selestine,Rwenyagira Alphonce,Dastan Buchard, Faswiu Athuman,Gozibert Arikad na Dezdery Everigist huku baadhi yao wakitoa machozi wakiwa mahakamani.
Miongoni mwa watuhumiwa hao,mshitakiwa namba moja ambaye ni padri Elpidius Rwegoshora tayari ameweka wakili wa kumtete ambaye anaitwa Mathias Rweyemamu.