Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Waziri Jerry Silaa kwa kazi nzuri aliyoifanya akiwa Waziri wa Ardhi ambapo amemtaka kwenda kuendeleza kasi hiyo kwenye Wizara yake mpya ya Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa kusimamia uhuru wa habari na kuwaunganisha Wananchi wa Mijini hadi Vijijini na mawasiliano.
Akiongea Ikulu Dar es salaam leo July 26,2024 baada ya kuwaapisha Viongozi mbalimbali, Rais Samia amesema “Nianze na Waziri Silaa umefanya kazi nzuri ndani ya ardhi pamoja na mawimbi ya hapa na pale lakini umetufanyia kazi nzuri na kuonesha kwa vitendo kwamba kero za ardhi zinatatulika, zile clinic zako za ardhi zimekuwa mfano mzuri wa kutatua kero hapohapo zinapozungumzwa”
“Wizara ya Habari ni muhimu sana katika utekelezaji wa ile falsafa yetu ya R4 na hapa nitagusia uhuru wa habari kwamba lazima uendelee kusimamiwa kikamilifu, hakuna uhuru usio na mipaka yake, nenda kashirikiane na Watu wa Sekta ya Habari hawa ni Watu muhimu sana kwa Taifa hili, Vyombo vyote vya Habari ni muhimu kwa Taifa letu”
“Kama tunavyojenga barabara kuunganisha Miji na Vijiji kwa kurahisisha mawasiliano hivyohivyo tunatakiwa kuwaunganisha Wananchi na mawasiliano ya simu kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa minara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), bahati mbaya yule sijui ndio Meneja au Mkurugenzi (Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Tumaini Mashiba), fagio lilimkumbuka lakini tutajitahidi kukuwekea mwingine mzuri, kwahiyo nenda kaimarishe mawasiliano”
“Lakini katika kujenga uchumi wa kigitali, nilitoa maelekezo mifumo ya Serikali kufikia December mwaka huu iwe inasomana, nenda kalisimamie hilo”