Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetambulisha rasmi huduma yake mpya ya wakala wa pesa kupitia benki ambayo inamruhusu mteja asie na akaunti ya benki hiyo kuweza kufanya miamala ya kifedha kwa kutumia kitambulisho chake cha taifa tu.
Ikitambuka kama ‘NBC Wakala Pesa’, huduma hiyo ya kwanza kutolewa na benki hapa nchini ni sehemu ya azma dhati ya benki hiyo katika kuwawezesha na kuchochea ujumuishi wa kifedha hapa nchini.
Uzinduzi wa huduma hiyo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika moja ya ofisi ya wakala Mkuu wa benki hiyo eneo la Manzese, Dar es Salaam, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki hiyo, Elibariki Masuke.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na maofisa wa benki hiyo akiwemo Meneja wa Huduma ya Uwakala wa benki hiyo, Jacquilen Sindano.
Akizungumzia huduma hiyo Masuke alisema inatoa nafasi kwa wateja wasio na akaunti kwenye benki hiyo au benki nyingine kuweza kuweka, kutoa, na kuhamisha fedha kupitia wakala wa NBC walioidhinishwa kwa kutumia vitambulisho vyao vya taifa au vya Ukaazi kwa upande wa Zanzibar.
“Kupitia huduma hii NBC tunatambua kuwa upatikanaji wa huduma za kifedha ni haki ya msingi ya kila Mtanzania bila kujali hadhi zao za kijamii na kiuchumi,” alisema Masuke. “Huduma yetu ya ‘NBC Wakala Pesa’ imebuniwa kuvuka vikwazo ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikizuia maelfu ya wananchi kutumia mfumo rasmi wa kifedha.”
Alisema huduma hiyo bunifu pamoja na kurahisisha mchakato wa miamala pia inachochea idadi kubwa ya wananchi kushiriki kwenye huduma rasmi za kifedha.
“Uzinduzi wa huduma hii ni ushuhuda wa azma dhati ya NBC ya ujumuishaji wa kifedha,” aliongeza Sindano. “Kwa kutumia mtandao wetu mpana wa mawakala nchini, tunaleta huduma za benki moja kwa moja kwenye milango ya wale ambao kwa kihistoria hawakuhudumiwa.”
Katika uzinduzi huo ilishuhudiwa wateja wakipata fursa kujifunza huduma hiyo moja kwa moja huku wakionyesha shauku na kufurahia urahisi mpya uliopatikana.
Nimekuwa mvivu kufungua akaunti ya benki kwa sababu ya kuhofia taratibu ndefu,” alisema Fatuma Ally, mkazi wa eneo hilo. “Lakini kupitia huduma hii ya ‘NBC Wakala Pesa’ sasa naweza kusimamia masuala yangu ya kifedha kwa urahisi bila kabla ya kufungua akaunti,”
Akizungumzia huduma hiyo Frank Maningi, Wakala Mkuu wa NBC eneo la Manzese alisema huduma hiyo inatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kihuduma kupitia benki kutokana na kugusa idadi kubwa ya Watanzania ambao bado hawajafungua akaunti za benki.
“Huduma hii ni mageuzi makubwa kwa jamii yetu. Inatoa njia salama na zaidi inajumuisha watu wengi zaidi kuingia kwenye huduma rasmi za kifedha hatua ambayo itawawezesha kufanya miamala kwa urahisi.” alisema.
Mwisho…