Waandamanaji wa Israel wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia walivamia kambi ya jeshi wakionyesha uungaji mkono kwa wanajeshi wanaotuhumiwa kumdhulumu vikali mfungwa wa Kipalestina.
Umati mkubwa wa watu ulikusanyika nje ya jengo la Sde Teiman baada ya polisi wa Israel kuingia humo kuwazuilia askari wa akiba, ambao sasa wapo chini ya uchunguzi rasmi.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa taarifa akilaani vikali tukio hilo na kutoa wito wa “kutulizwa kwa hasira mara moja”.
Waandamanaji pia walivunja kambi ya pili ya kijeshi, ambapo askari wa akiba walipelekwa kuhojiwa, lakini msemaji wa polisi alisema maafisa waliweza kutuliza hali
Wapalestina waliokuwa wakizuiliwa na Israel wakati wa vita vya Gaza kwa kiasi kikubwa walishikiliwa kwa siri na katika baadhi ya matukio walitendewa kiasi cha mateso, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesema siku ya Jumatano Julai 31, 2024.
“Ushuhuda uliokusanywa na ofisi yangu na watu wengine huandika mfululizo wa vitendo vya uhalifu, kama vile kuzamishwa majini na kuwaachilia mbwa wafungwa, miongoni mwa mambo mengine, kinyume cha sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu.” amesema Volker Türk.
Takriban wafungwa hamsini na watatu kutoka Gaza na Ukingo wa Magharibi wamekufa wakiwa kizuizini nchini Israel tangu Oktoba 7, 2023, kulingana na ripoti ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ambayo inaangazia kipindi cha kuanzia Oktoba 7 hadi Juni 30.
Tangu shambulio la Hamas katika ardhi ya Israel tarehe 7 Oktoba, maelfu ya Wapalestina – ikiwa ni pamoja na madaktari, wagonjwa, wakaazi na wapiganaji waliotekwa – wamechukuliwa kutoka Gaza kwenda Israeli, “kawaida wakiwa wamefungwa pingu na kufungwa macho,” na maelfu ya wengine walifungwa katika Ukingo wa Magharibi na Israel, ripoti inasema.