Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa (BMH) imekuwa ya kwanza nchini kutoa Huduma ya upandikizaji uloto kwa mgonjwa wa sikoseli ambaye anatofautiana kundi la damu na mchangiaji wake na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutoa huduma hii.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Damu BMH ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dkt. Stella Malangahe leo Julai 30, 2024 Jijini Dodoma mara baada ya kufanya upandikizaji uloto kwa mgonjwa wa sikoseli ambaye anatofautiana kundi la damu na mchangiaji wake wa uloto.
Dkt. Stella amesema Hospitali ya Benjamini Mkapa kupitia kitengo chake cha Damu Salama sasa kina uwezo wa kuchakata uloto uliotolewa na mchangiaji mwenye kundi tofauti la damu na mpokeaji (mgonjwa) na hivyo kupandikizwa bila kuleta madhara yoyote katika mwili.
Dkt.Stella amesema kuwa Utaalam huu unaojulikana kama Bone Marrow Manipulation- RBC Depletion ni utaalam unaofanywa na mashine maalum (Apheresis machine) kwa kuchuja na kuchukua Uloto ulio kusudiwa kisha kumpandikiza uloto uliobakia.
“Mgonjwa huyu aliyepandikizwa pamoja na mchangiaji wake wanaendelea vizuri na tayari mgonjwa huyu ameonesha dalili nzuri za kuotesha uloto. Mwanzoni tulipoanzisha huduma hii ya upandikizaji uloto hatukuweza kupandikiza uloto kwa mgonjwa mwenye sikoseli anayetofautiana kundi la damu na mchangiaji wake, lakini sasa kupitia utaalam huu tunaweza kupandikiza uloto kwa wagonjwa ambao wachangiaji wao wana makundi tofauti ya damu” amesema Dkt. Stella
Dkt. Stella ameeleza vigezo vingine wanavyozingatia katika upandikizaji uloto mbali na kundi la damu, ambapo kwa sasa limepatiwa ufumbuzi ni pamoja na umri wa mgonjwa (miaka 4 hadi 12), uwepo wa mchangiaji uloto mwenye ufanano wa kina saba na mgonjwa (HLA matching) na hali nzuri ya afya ya mgonjwa na mchangiaji uloto.