Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Mawakili kusimamia Haki na Amani nchini ili kuhakikisha haki inatendeka kwa watu wote ili kuchochea maendeleo.
Dkt. Biteko ametoa wito huo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wanansheria Tanganyika (TLS) kinachoendelea Jijini Dodoma.
” Amani ili iwepo ni lazima haki ionekane ikitendeka kwa maana kwamba haki huleta amani na amani huleta maendeleo kwa nchi yetu,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema TLS wakati inaadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, wanachama wake wanatakiwa kutafakari mwelekeo wa chama hicho kitaaluma ili kuendana na azma ya Serikali ya awamu ya sita ambayo imeweka nia thabiti katika kuhakikisha haki inaonekana ikitendeka.
“Tumieni muda kusema na kusikiliza hoja za watu wanaojua na wasiojua kwa kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kuna heshima mahala pa kazi”. alisema Dkt. Biteko
Aidha Dkt. Biteko amewataka wanachama wa TLS kutumia taaluma yao kushikriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwakani.
Awahimiza kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuleta maendeleo badala ya kuzingatia tofuati nyingine zinazowatofutisha binadamu.
Akizungumzia uchaguzi ndani ya TLS, Naibu Waziri Mkuu amewataka wajumbe kuchaguana kwa kuzingatia vigezo nia na mwelekeo wa wagombea watakao kiwezesha chama hicho kusonga mbele na siyo wale wanaotanguliza maslahi binafsi badala ya chama.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameipongeza TLS kwa ushirikiano na taasisi za elimu na taasisi rafiki na TLS kuhakikisha Wananchi wanapata haki kwa wakati.
Amesema Wizara imeanzisha namba maalum inayotumiwa na watu wote kuwasilisha hoja na kuomba ushauri wa kisheria suala linalorahisha upatikanaji wa haki.
Naye, Rais wa TLS Wakili Harold Sungusia amesema kwa sasa katika kitabu cha orodha ya mawakili kuna idadi ya mawakili 12,471 kwa ongezeko hili Watanzania watapata fursa nyingi ya kuhudumiwa na mawakili hawa nchi nzima ili kutatua changamoto zilizopo za kisheria.
“ Vitendo vya kukamatwa kwa mawakili hadharani wakati wakiwakilisha wateja wao vimepungua sana ikilinganishwa na miaka iliyopita, tunatamani useme neno mheshimiwa mgeni rasmi ikiwezekana kwa kuwa ni aibu wakili kushikwa Tanganyika Jeck akiwa kazini” amesema Sungusia.
Aidha amepongeza falsafa ya R4 za Mheshimiwa Rais ambazo amesema zimechangia katika kuboresha uhusiano kati ya Wanasheria na mifumo ya usimamizi wa sheria nchini.