Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imewakumbusha wanafunzi wanaoomba mkopo wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2024/2025 kusoma miongozo na kuizingatia ili kuepuka kuwasilisha maombi yenye makosa.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema hayo leo (Alhamisi, Agosti 1, 2024) kuwa tathmini ya siku 60 zilizopita inaonesha maombi yanayowasilishwa hayazingatii miongozo iliyotolewa.
“Dirisha la kuomba mkopo kwa njia ya mtandao kwa makundi mbalimbali lipo wazi kwa siku 90 kuanzia Juni 1 mwaka huu … na tumepokea zaidi ya maombi 40,000 lakini yaliyo kamili ni chini ya 25,000 … tunashauri waombaji wasome miongozo inayopatikana katika tovuti yetu (www.heslb.go.tz),” amesema Dkt. Kiwia.
Kuhusu ‘Samia Skolashipu’ kwa 2024/2025
Kwa waombaji wa Skolashipu za Samia ambazo zinawalenga wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika mitihani ya kidato cha sita, Dkt. Kiwia amesema orodha ya wanafunzi hao itaanza kupatikana katika tovuti ya HESLB kuanzia kesho, Ijumaa, Agosti 2.
“Tumeshapokea orodha ya wanafunzi 700 wenye ufaulu wa juu kutoka kwa Wizara yetu, tunakamilisha utaratibu waweze kuomba fursa za ‘Samia Scholarships’ kuanzia keshokutwa, Agosti 3,” amesema Dkt. Kiwia.
Kuhusu fursa za BURE za mafunzo ya kuongeza ujuzi
Aidha, Dkt. Kiwia amewakumbusha wanafunzi-wahitimu na waliopo mwaka wa mwisho wa shahada za TEHAMA na sayansi ya kompyuta (ICT and Computer-related degrees) kutumia siku nne zilizobaki kujisajili na kuomba fursa za mafunzo kupitia https://dlt.adanianlabs.io.
“Tuna makubaliano na taasisi ya Adanian Labs ili kutoa mafunzo ya bure kwa njia ya mtandao kwa wanufaika wetu ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa … watumie siku nne hizi kujisajili na kupata fursa za mafunzo,” amesema Dkt. Kiwia.
Kuhusu Bajeti ya Mikopo
Katika mwaka wa masomo 2024/2025, Serikali imetenga TZS 787 bilioni ambazo zinatarajiwa kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 245,000 wakiwemo wanafunzi 80,000 wa mwaka wa kwanza.
Katika mwaka wa masomo 2023/2024, Serikali imetoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi 224,056, wakiwemo wanafunzi 78,979 wa mwaka wa kwanza.