Bwana la Mindu lililopo Manispaa ya Morogoro linategemewa kwa zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wa Morogoro katika upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wakazi wa Manispaa hiyo ambapo wadau na Serikali wamekua wakisisitiza utunzwaji wake Ili wananchi kuwa na uhakika wa huduma ya maji.
Katika kuendelea na mikakati hiyo hapa unafanyika uzindua rasmi utekelezaji wa Mradi wa Uhifadhi na Ulinzi wa Bwawa la Mindu unaotekelezwa kwa mashirikiano kati Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu na MORUWASA chini ya ufadhili wa World Water Worx unaogharimu zaidi ya kiasi cha Shilingi Bilioni 2 ikijumuisha mchango wa serikali na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili.
Akizundua Mradi huu Katibu tawala Mkoa Morogoro Dokta Mussa Ally Mussa anasema Mradi unalenga kulinda na kuhifadhi mazingira ya eneo la Mindu ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira ambapo utekelezaji wa mradi huu utahusisha hatua mbalimbali za uhifadhi na Urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa na shughuli mbalimbali za kibinaadamu hasa kilimo na ufugaji.
Dkt. Mussa amesisitiza suala la Ushirikishwaji wa jamii katika ulinzi wa vyanzo vya maji kwa kuwaletea miradi itakayokwenda kuondoa umasikini na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Idara ya Rasilimali za Maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Bw. Martine Kasambala ameanisha maeneo makuu manne ambayo yanaenda kufanyika kupitia mradi ikiwemo kuendeleza Kilimo Misitu, Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Kaboni, Kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Sekta binafsi katika uhifadhi wa vyanzo vya maji pamoja na kujenga uwezo kwa jamii kwa kutoa mafunzo maalumu ya kuishi rafiki na mazingira.
Chanzo cha maji cha Bwawa la Mindu ndio tegemeo kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwa ndio chanzi kikuu cha maji safi kwa zaidi ya 75% kwa matumizi ya majumbani huku likiwa na ukubwa wa eneo takribani kilomita za mraba 303 lenye mito mikuu 5 inayolisha Bwawa hilo ambayo ni Ngerengere, Mgera,Malali,Mzinga na Lukulunge.