Wimbi la maandamano bado linaendelea kushamiri barani Africa na kwingineko ambapo pia nchini Nigeria Mamia ya watu waliingia barabarani katika miji kadhaa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, wakitaka serikali ichukue hatua za kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha, jambo ambalo linalaumiwa kwa kiasi kikubwa na sera za kiuchumi za Rais Bola Tinubu, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya muda mrefu ya mafuta na kushusha thamani ya fedha ya nchi.
Polisi imesema takriban watu wanne waliuawa na wengine 34 kujeruhiwa baada ya kilipuzi cha kutengenezea kulipuliwa katika umati wa watu waliokuwa wakipinga hali ngumu ya kiuchumi katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno siku ya Alhamisi.
Kulingana na taarifa ya Inspekta Jenerali wa Polisi, Kayode Egbetokun, iliyochapishwa kwenye X, majeruhi 34 walikuwa kwenye “orodha ya hatari.”
Polisi pia walisema ”wafanya ghasia” walimuua afisa mmoja wa polisi katika Jimbo jirani la Gombe na kwamba kilipuzi kilipatikana bila kulipuka katika mji wa kusini wa Lagos, kitovu cha biashara nchini humo.
Mamlaka zinasema waandamanaji hao walishambulia vituo vya polisi katika miji kadhaa, huku waandamanaji hao wakishutumu vikosi vya usalama kwa kuwafyatulia risasi.
Serikali siku ya Jumatano iliorodhesha misaada ambayo imetoa ili kupunguza maumivu ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuongeza viwango vya chini vya mishahara, kupeleka nafaka katika majimbo kote nchini, na misaada kwa wanaohitaji zaidi.