Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imeipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kusimamia kanuni za usalama wa mizigo na usalama wa utendaji kazi wa bandari na bandari kavu hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo, Mhe. Dkt.Jason Rweikiza (Mb) leo tarehe 02 Agosti,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya kamati hiyo kutembelea TASAC.
“Sisi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo tumefurahi na kuona udhibiti unaotolewa na TASAC katika kusimamia kanuni hiyo unatekelezwa na wadau vizuri,” alisema Mhe. Dkt. Rweikiza.
Kamati hiyo imefanya ziara ya kutembelea ofisi za TASAC zilizopo jengo la SUMATRA , Bandari kavu za PMM 2001 “Limited”, GALCO, TRH na gati namba 8 hadi 11 ya meli za makasha zinazohudumiwa na Tanzania East A frica Gateway Terminal Limited (TEAGL), gati namba 0 hadi 7 yanayoendeshwa DP World.
Aidha, Kamati imeweza kupokea maoni ya wadau wanaodhibitiwa na TASAC na kueleza kuwa TASAC wanafanya kazi vizuri na ni wasikivu wanapowasilisha changamoto zao kila zinapojitokeza.
“Inapotokea changamoto yoyote TASAC ukaa pamoja na sisi na kuitatua kwa haraka,” amesema Bw. Mathew Clift, Afisa Mkuu wa Fedha wa DP World.
Aidha, Bw. Clift amesema DP World kwa muda miezi minne tangu waanze kutoa huduma bandarini wameweza kuhudumia meli kwa wakati na kupelekea kupunguza muda wa meli kusubiri kuingia gatini kutoka siku 30 hadi siku 7 tu. Hali hii imepelekea kupunguza gharama kwa mlaji wa mwisho na kuongeza shehena na mapato ya nchi.
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe.David Kihenzile amesema kuwa kamati hiyo hupitia kanuni zinazosaidia utendaji kazi za udhibiti na kupelekea bandari kutoa huduma bora na salama katika bandari zetu.
“Leo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imefanya ziara ofisi za TASAC, Bandari kavu na hatimae Bandari ya Dar es Salaam. Katika ofisi za TASAC wamepitishwa kwenye wasilisho la Kanuni ya Ulinzi na Usalama wa Mizigo katika maeneo ya Bandari na Bandari kavu,” amesema Mhe. Kihenzile.