Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema Serikali inajenga miradi ya maji 8 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 15 kwa lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa majisafi katika Wilaya ya Mvomero.
Pia Kwa eneo la Dakawa mjini amesema kuna mradi wa uboreshaji huduma ya Maji wa kiasi cha Bilion 2.3 ambapo tayari Mkandarasi amepokea malipo ya awali.
Waziri Aweso ameyasema hayo leo hii katika Ziara ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkoani ambapo amebainisha kuwa kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji kwa wilaya ya Mvomera ni asilimia 68.5 ambapo mara baada ya kukamilika kwa miradi hiyo upatikanaji wa maji utafikia aslimia 86.
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso akijibu hoja ya Mbunge wa Jimbo la Mvomero ameeleza kuwa mradi wa Visima Virefu vinavyochimbwa eneo la Mkata well Field vikiwa visima vikubwa vya kwanza ndani ya Mkoa Morogoro vinavyochimbwa kujiridhisha juu ya uwepo wa Maji chini ya Ardhi ambapo Upatikanaji wa Maji ya uhakika eneo hilo itakua ni chanzo mbadala cha Maji kwa mji wa Morogoro kama ilivyo eneo la Mzakwe Dodoma na kusema baada ya kukamilika Mradi huu eneo la Dakawa-Mvomero litapewa kipaumbele kabla ya Maji kupelekwa Morogoro mjini.