Wakikaidi ukandamizaji mbaya na amri ya kitaifa ya kutotoka nje, waandamanaji nchini Bangladesh wametoa wito wa maandamano makubwa kuelekea mji mkuu Dhaka.
Vikundi vya wanafunzi vilivyokuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo vilihimiza kuzingirwa kwa mji mkuu siku ya Jumatatu. Wito huo unaibua mvutano zaidi kufuatia ghasia mbaya siku ya Jumapili ambazo zilisababisha karibu watu 100 kuuawa na kutangazwa kwa amri ya kutotoka nje ya kitaifa.
Maandamano yaliyoanza mwezi uliopita kuhusu nafasi za kazi za serikali yameongezeka na kusababisha machafuko ya kitaifa huku kukiwa na ukandamizaji wa mamlaka. Waandamanaji sasa wanamtaka Waziri Mkuu wa muda mrefu Sheikh Hasina ajiuzulu.
“Maasi haya ya wanafunzi yataendelea hadi kuanguka kwa Sheikh Hasina,” mratibu wa maandamano Asif Mahmud alisema katika ujumbe kwenye Facebook jioni ya Jumapili. “Kesho ni ‘Machi hadi Dhaka’. Safiri hadi Dhaka sasa ili ushuhudie historia. Jiunge na pambano la mwisho,” alisema.
Ghasia hizo hadi sasa zimesababisha vifo vya karibu watu 300, na hali ya wasiwasi ilikuwa ikiendelea huko Dhaka siku ya Jumatatu, baada ya mamlaka kutangaza amri ya kutotoka nje usiku wa kuamkia leo.
Vifaru vya jeshi na magari ya polisi yalikuwa mitaani na vikosi vya usalama vilishika doria kwa miguu, kituo cha habari cha mtandaoni kilionyesha. Kulikuwa karibu hakuna trafiki ya kiraia, ukizuia pikipiki chache na teksi za magurudumu matatu.